Saturday 8 February 2014

THESUSE NA JITU MINOTA



Thesuse na mama yake, Athera, waliishi chini ya mlima mkubwa mahali palipoitwa Trozeni. Thesuse alipokuwa angali mchanga baba yake, Egesu, aliinua jiwe kubwa lililokuwa mlimani katikati ya msitu na hapo alilaza upanga na sapatu chini yake. kisha akamuambia Athera kuwa Thesuse atakapokuwa mkubwa na mwenye nguvu za kuinua jiwe hilo basi amfuate kule Atheni –huko Egesu alikuwa mfalme wa Attika.


Thesuse alipokuwa mkubwa, aliweza kuchomoa ule upanga na sapatu kutoka chini ya jiwe na akafunga safari kuelekea Atheni. Safari ya kuelekea Atheni haikuwa rahisi, ilikuwa na misitu mengi na nyuma ya mawe makubwa walijificha majitu na majambazi. Lakini, Thesuse alimuaga mama yake na kujaribu bahati yake. Hata hakuwa ameenda mbali sana alipovamiwa na Perifite –aliyejulikana kwa utani kama “mbeba rungu.”  Alionekana jamaa wa kutisha sana akiwa na amebeba hiyo runga yake kubwa ya chuma. lakini Thesuse alimkabili na muda si mrefu alikuwa amemwangamiza hapo barabarani. Akachukua hata hiyo rungu yakena kuendelea na safari.


Mbele zaidi alikutana na Sinusi “mkunja miti.” Ukatili wake ulikuwa wa kuwararua wasafiri kwa kuzinyambua miti mbili kubwa na kisha kufunga msafiri kwa miti hizo na kuziwachilia zinepuke na kumrarua mtega nyara huyo. Sinusi mwenyewe alikuwa pia na runga lakini haikuwa na nguvu kama ile Thesuse alikuwa amebeba. basi siku hiyo ilikuwa Sinusi aliyeraruliwa na miti hizo zenye mnaso. Akiendelea na safari alikutana na jambazi aliyeitwa Sironi ambaye alilazimisha wasafiri wamwoshe mikuu hatimaye aliwapiga teke na kuwaangusha kutoka ngomeni hadi baharini. lakini wakati huu ilikuwa Sironi aliyepokea adhabu hiyo. Mbele kidogo paliishi jambazi mwingine kwa jina Porokruste ambaye alijifanya kuwa mtu mkarimu na kuwakaribisha wageni kwenye chumba chake lakini, wakipatikana kuwa  warefu kuliko kitanda chake, aliwakata vichwa au mikuu hadi watoshee. Na, wakiwa wafupi, aliwavuta shingo na miguu hadi waliporefuka na kutoshea kitanda hicho. lakini pia Porokruste alipata adhabu yake kama tu wale majambazi na majitu waliyomtangulia kwenye hii safari ya kuelekea Atheni.


Wakati huo mrembo Medai ambaye pia alikuwa mlozi mkubwa alikuwa akiishi kwenye ikulu ya mfalme. Alikuwa na mtoto kijana aliyemtarajia kumridhi mfalme Egesu kwa hivyo alimtengenezea Thesuse kinywaji kilichojaa sumu na kumwandalia kwenye kikombe kikubwa. Alimwambia mfalme kwamba mgeni huyo wake alikuwa mkora ambaye alikuwa amekuja tu kumpokonya ufalme wake na hivyo akamshawishi mfalme ampe Thesuse kinywaji hicho. Thesuse hakujua njama hiyo na alikuwa ameshainua kikombe ili akunywe kinywaji wakati Egesu alipoona ule upanga wake pamoja na sapatu na akakumbuka mwanawe. Aliruka na kukichukua kikombe hicho chenye kinywaji hatari, na akakitupa mbali.

Medai alitumia mbinu zake na akafaulu kujiponya na kutoroka. kwanza allita uchusichusi kutoka mtoni ukamfunika. Kisha akaiita majitu yake yaliokuwa na mabawa na akaruka kwa gari ambalo majitu hayo yaliivuruta na akatoroka Atheni- asirudi tena. Watu nao hawakuchelewa kumweleza mfalme sifa zote za ujasiri wa Thesuse ambazo alizionyesha katika safari yake kutoka Trozeni hadi kifika kwake Atheni. Egesu alifurahia sana ngano hizo hata akatangaza siku tatu za kusherekea kuwasili kwa Thesuse. Lakini kwenye hiyo harakati, alikuja mjumbe mmoja kutangaza kwamba wale wawia kutoka Krete wamewasili.


Ilitokea kwamba hapo zamani, mwana na mridhi wa mfalme Minoso wa Krete aliuawa na Waatheni. Na kulipiza kitendo hicho, mfalme Minoso aliwashambulia Waatheni kwa kikosi chake kikubwa cha jeshi na kuwalazimu Waatheni kukubali masharti yake ambayo yalikuwa kwamba kila baada ya miaka tisa watampa ‘watoto wa kafara’ ambao walikuwa wanaume saba na mabinti saba. Naye aliwachukua hao ‘watoto wa kafara’ na kuwatupa kwa jitu moja kubwa liloitwa Minota ambalo ingawa kiwiliwili chake kilikuwa cha mtu, kichwa chake kilikuwa cha fahali. Minota aliishi pangoni huko Krete Karibu na ikulu ya mfalme. Pango hilo lake lilikuwa na njia nyingi ambazo zilimchanganya yeyote aliengia humo. Hakuna hata mtu mmoja aliyefaulu kurejea kutoka humo pangoni mara tu alipoingia.


Thesuse aliamua kwamba ataangamiza jitu hilo na kukomesha dhuluma hiyo duni ya kuwaua watu kumi na wane wasio na hatia kila baada ya miaka tisa. Na basi, hata kabla ya kuchaguliwa wale vijana ambao wangepelekwa Krete, Thesuse alijitolea muhanga na wale wengine wakachaguliwa kwa kupigiwa kura kama ilivyokuwa desturi. Jambo hilo la Thesuse kujitolea kivyake lilimletea umaarufu sana mbele za watu. Muda si muda, merikebu iliyowabeba watoto hao wa kafara ilinoa nang’a huku imevikwa tanga ya rangi nyeusi kama ilvyokuwa kawaida ila wakati huu mfalme Egesu alimpa mwanawe tanga ingine nyeupe ili aipeperushe kwa merikebu kama atakuwa bado hai wakati wa kurejea.
Walipowasili Krete Thesuse hakuchelewa kumweleza mfalme Minoso kwamba nia yake ilikuwa Kumuua jitu Minota. Minoso alikubali ombi la Thesuse kwamba akifaulu basi yeye na wale wanakafara wengine wataachiliwa huru na tena deni lake litakuwa limelipwa milele. Hata hivyo, Minoso aliongeza sharti kwamba Thesuse ataingia mle pangoni bila upanga wake kuenda kukabiliana na jitu. 


Hapo kwa dari ya chumba ambacho walikuwa wamefungiwa Thesuse na wenzake palikuwa chumba cha binti zake mfalme Minoso, Ariadin na Faidera ambao waliamua kumsaidia Thesuse katika juhudi zake. Walifungulia Thesuse mlango kama wale wengine bado wamelala na kumpeleka hadi palipokuwa hiyo pango maarufu lenye kuta za marumaru zilizong’a kwenye mwangaza wa mwezi. Ariadin alimfichulia “Wakati huu ndiyo mzuri wa kuua jitu hilo kama lingali linalala. Usiongojee hadi asubuhi likishaamka” Ariadin aling’ong’oza. “Maskani yake ni humu katikati mwa pango hili lenye njia nyingi zenye mikato aina ya labiranthi. Fuata sauti ya mg’oroto wake. Pia chukua upanga huu na kipira cha uzi ambao utatumia kupata njia ya kurejelea kutoka pangoni” Kwa hayo maneno, ariadin alibaki kama ameushika mwanzo wa uzi na Thesuse akaingia na mradi wenyewe akiachilia polepole kwa kuelekea ndani, upanga nao thabiti mkononi.


Mle ndani njia zilikuwa kabibu na nyingi zilikuwa na wa mkingo wa gafla bila kuelekea popote na hapo Thesuse ilimbidi arudi nyuma na kutafuta tena. Inasemekana kuwa hapajawai kuwa na mikato za labirathi zilizokuwa za kutatiza kama hizi zilizotengenezwa na mhandisi Dadesulu. Ingia ndani, toka tena; ingia Thesuse aliendelea. Alizidi kusikia sauti ya kung’orota kwa Minota ikiongezeka na kujua kwamba anakaribia makao yake. Kwa hayo yote Ariadin na Faidera waliongojea langoni, Ariadin akishikilia upande wake wa uzi kwa ustadi. Mara walisikia mtetemeko mkubwa na yowe kwa mbali kisha kukawa na kimya kikuu. Ariadin hangeweza kujua kama Thesuse ameuawa au kama hata bado alikuwa na ule mradi ulioviringishwa uzi lakini alianza kuhisi uzi ukivutuavutua halafu muda si mrefu mwana wa mfalme Egesu akajitokeza.


Ile meli iliyowaleta Thesuse na wenzake Krete ilikuwa bado pale ufuoni. Vijana walikuwa wangali wanalala walipoamshwa na mara moja walikuwa safarini kurudi Atheni. Nao pia Ariadin na Faidera kwa kuhofia hasira ya baba yao, waliwafuata. Katika safari hiyo walitua kwenye kisima cha Nakso na wakatengeneza kambi hapo kwa miamba usiku. Kesho yake asubuhi na mapema waliendelea na safari hiyo yao lakini Ariadin alibakia kama amelala na kwa hivyo aliwachwa nyuma. Thesuse hakusahau tu Ariadin ila pia kupeperusha ile tanga nyeupe baba yake alikuwa amempa. Kwa hivyo meli yao ilipojitokeza Atheni na tanga nyeusi juu yake mfalme Egesu alijitupa baharani akidhani kuwa mwanawe hakufaulu.


 * Ariadin alichukuliwa na Bachisu akampeleka angani na kumvisha taji iliyo na nyota tisa kichwani. Yeye huonekana hadi leo angani ya kaskazini.

No comments:

Post a Comment