Sunday 11 December 2011

TABARUKU: BURIANI KWA SAMUEL MUSHI

Mwaka huu umekuwa na hasara zake. Juu ya kutupokonya Profesa Maathai hapa Kenya, umetunyanganya mwana-lugha mkuu na mkongwe ambaye kuaga kwake bila shaka ni hasara kubwa kwa jumuia na wazalendo wa Kiswahili na hasa fani ya fasihi. Tarehe 23 Julai mwakani, mwalimu Samuel Mushi alipiga dunia teke na akaenda zake mbinguni. Alifariki alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali mmoja inayofahamika kama Muhimbili National Hospital huko Tanzania. Alikuwa na miaka sabini na miwili (alizaliwa 1939). Hata hivyo, jambo la muhimu ni kuwa alifanya mchango wake na sasa waliobaki nao wafanye yao.
Wengi labda hawamfahamu mwalimu Mushi kwa jina, hasa hapa Kenya, lakini wengi wameshasikia hadithi ya mfalme Edipode ambayo mwalimu huyu aliitafsiri mnamo mwaka wa 1971. Hadithi hiyo, baada ya kutafsiriwa na mwalimu Mushi, ilivuma sana na kuwafikia watu wengi ambao hawangepata fursa ya kuisikia kwa vile wangetatizwa kuielewa katika hati za lugha za kimombo. Ufanisi huo ulikuwa hakikisho tosha kwamba fasihi haina mipaka na hamu ya wanadamu wote kusimuliwa hadithi nzuri ipo. Pia hadithi yoyote ile yawezafikia kila mtu, bora mbinu za kuieneza na kueleza ziwe mwafaka.
Hadithi bila shaka ilikuwa ya Sophocles ambaye tunamwita Sofokile, ila mwalimu Mushi aliipa msisimko wa Kiswahili hata kuifanya ionekana ngano ya hapa nyumbani na wala si ya ughaibuni. Lakini, hiyo sio kazi pekee aliyoifanya mwalimu huyu. Hata kabla ya kuswahilisha Sophocles, alikuwa ameshaswahilisha William Shakespeare -mchezo wa Makbeth akiwa na umri wa miaka 29 tu, na Tufani mwaka mmoja baadaye (1969). Hata hivyo tamthilia hizo hazikufana sana Kenya kwa kufuatia maudhui yao ambao yalilenga sana ushirikina. Kazi hizo alizifanya labda akifuata katika nyayo za mtangulizi wake -Mwalimu Nyerere, ambaye alikuwa amekwishaswahilisha Juliasi Kaizari (1963).
Katika ustadi wa utafsiri fasihi huenda Mushi alimpiku mwalimu Nyerere. Sababu ya kunawiri kwa Mushi kushinda Nyerere (kwa mtazamo wangu) ni kwamba huyu wa pili aliegemea sana fasihi ilihali huyo wa awali aliegemea sana siasa. Mushi alitafsiri akiwa na nia na kutumbuiza na kuongozwa na uhondo wa fasihi, yaani aliwasilisha pamoja na kuwakilisha. Mwalimu Nyerere naye alitamani sana kuangazia maswala ya kisiasa yaliyomo kwenye maandiko husika. Ndipo hata katika tafsiri yake ya "Things Fall Apart" mwalimu Nyerere aliipa mtazamo wa "Shujaa Okonkwo" badala ya "Dunia Imepasuka." Nyerere aliendelea kumwona Okonkwo kama shujaa, ingawa fasili inamtambua kama mtu hafifu.
Ni bayana pia Mushi alichagua hadithi zenye rutuba kubwa ya kifasihi kushinda wengi waliomtangulia. Ingawa hivyo si kusema kuwa hapawezijitokeza mwandishi mwingine akazisimulia kazi hizo na zinginezo kwa ubora kumshinda. Hata mwenyewe alikiri katika utangulizi wa Tufani kwamba "...napenda kusema kama ikiwa upungufu wa tafsiri yangu utauudhi baadhi ya wasomaji kiasi cha kuamsha cheche za shauku ya kutoa tafsiri nzuri zaidi ya mchezo huo au kuifuatisha hadithi ya mchezo huo kwa ukamilifu zaidi...hakuna atakayefurahi kunishinda."
Mchango wa Mushi kwa fasihi haukukomea hapo kwa vile ni yeye aliyekuwa na ujasiri mkubwa kutohoa na kubuni majina mengi ambayo hayakuwepo kabla yake, hasa katika msamiati wa fasihi ya kutafsiriwa. Hakuokopa kumwita Zeus- Zeo, Sophocles- Sofokile, Oedipus- Edipode, na Thebes- Thebe. Msamiati huu unasaidia sana wandishi wa badaye kuandika kwa upesi zaidi bila kusumbuliwa ama kusumbuka kubuni majina mapya kuzungumzia mambo au watu wale wale. Kwa wale ambao wamejaribu kuandika au kuzungumzia fasihi hizo kama Dkt. Richard Wafula (na mimi pia) wanafamu na kufaidi mchango huo wa Mushi kwa makini.
Mushi alipanua mipaka ya utungaji mashairi. Kwa kutafsiri Edipode akitumia mizani sita badala ya nane ama kumi na sita, amekomboa wandishi wengi ambao walikuwa wamefungiwa katika kanuni ambazo wakati mwingine hazitoshelezi tafsiri kikamilifu. Ingawa Stephen Mushi alichangia pia katika uandishi wa mambo mengine kama siasa (vitabu thelathini na moja hivi) lakini, ni kwenye nyanja ya fasihi ambapo nyota yake inang'a na haina mpizani wa dhati. Jinsi tu vile riwaya ya Kusadikika ya Shabaan Robert bado inashikilia upeo kama fasihi bora ya kiasili ndivyo tamthilia ya Mfalme Edipode ya Samuel Stephen Mushi inashikilia nafasi hiyo ya kuwa fasihi- tafsiri bora kufikia leo.
Kumalizia, mimi kama shabiki wa mwenda zake, nimemtugia Mushi shairi lifuatalo

Ulikichukua Kiswahili
Ukakiinua kikawa ni
Lugha ambayo
Ina hadhi ya kimataifa
Ina mengi ya kujivunia
Chombo ambacho
Chawezaelezea chochote
Chaweza kuchambua lolote
Msingi ulio
Imara kueneza fasihi
Bora kuendelezea kazi

Kwaheri mwalimu.
Edwin Musonye
(Edwin Musonye ni shabiki wa fasihi na lugha)
//